ON POINT MEDIA

ON POINT MEDIA
Karibuni sana kwa kazi nzuri ya video za harusi mikutano na kadharika

SHIRKA LA NYUMBA LA TAIFA

SHIRKA LA NYUMBA LA TAIFA
NYUMBA YANGU MAISHA YANGU

Friday, 21 October 2016

SHULE YA SEKONDARI KUSUNGU YA ILALA YAPOKEA VITI KUTOKA TPDC

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi viti 142 vyenye thamani ya shilingi milioni 6 katika Shule ya Sekondari Kisungu iliyopo kata ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam. 

Meneja Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu akikabidhi viti hivyo kwa niaba ya Mkurungezi Mtendaji wa TPDC amesema viti hivyo vitasadia kutatua changamoto ya wanafunzi kukosa viti shuleni hapo. 

Amengoze kuwa mchango huo wa viti ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia. 

Shirika hilo limekuwa na utaratibu wa kuchangia jamii katika nyaja za afya, elimu, maji, utawala bora na michezo kupitia programu yake kuwajibika kwa jamii.
Mkuu wa shule ya Sekondari Kisungu, Mkama Mgeta (kulia) na wanafunzi wa Shule ya Sekondari wakipokea kiti kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu (kushoto) katika hafla fupi ya kupokea viti 142 kutoka TPDC.
 Meneja Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC katika hafla fupi ya kukabidhi viti 142 vyenye thamani ya shilingi milioni 6 katika kwa Shule ya Sekondari Kisungu iliyopo kata ya Kinyerezi jiji Dar es Salaam.
 
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisungu, Philimina Casimr akisoma taarifa ya Shule hiyo kabla ya kupokea viti kutoka TPDC.
 Sehemu ya viti 142 vilivyotolewa na TPDC.

PROFESA Sospeter Muhongo Afunguka Kuhusu Madini Kuchangia Pato la Taifa Kwa Asilimia 10

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hadi kufikia mwaka 2025, sekta ya madini nchini inapaswa ichangie asilimia 10 kwenye Pato la Taifa.

Katika kipindi cha mwaka 2015 sekta hiyo imechangia asilimia 4.3 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka 2014, kiasi ambacho waziri huyo amesema bado ni kidogo.

Aliyasema hayo mjini Dodoma jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akitoa taarifa kuhusu shughuli za utafutaji madini na maendeleo ya sekta ya madini.

Hata hivyo, alitaja changamoto zinazoifanya sekta hiyo kuwa na mchango mdogo katika Pato la Taifa kuwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya madini kwenye soko la dunia na kutokuanzishwa kwa migodi mingine mikubwa ya uchimbaji hivi karibuni.

Alisema kwa sasa uwezo wa uzalishaji wa dhahabu kwa migodi yote nchini ni wakia milioni 1.25 kwa mwaka na uzalishaji kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 ni wakia milioni 5.68 sawa na tani 176.7 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 9.06 sawa na Sh trilioni 19.7.

Waziri huyo alifafanua kuwa ipo mipango mbalimbali ya kuendeleza shughuli za madini nchini ikiwemo kuboresha ukusanyaji na usambazaji wa taarifa na takwimu za kijiosayansi, udhibiti wa utoroshwaji wa madini na ukaguzi katika shughuli za uzalishaji madini.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche alitaka kujua hatua zinazochukuliwa dhidi ya tuhuma za utoroshaji wa madini unaofanyika katika baadhi ya migodi ikiwemo mgodi wa Accacia ambao ndani ya mgodi kuna kiwanja cha ndege. 

Serikali Yapunguza Deni La Mifuko Ya Hifadhi Ya Jamii


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7 kati ya sh. bilioni 964.2 za madeni ya michango ya jumla ambayo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa wadau wa NSSF ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600.

Amesema sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015 hadi kufikia sh. trilioni 10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016, takwimu zinaonesha idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia milioni 2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia shilingi trilioni 10.28 na mafao yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Juni 2016 ni shillingi trilioni 2.93. Michango ya wanachama kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15 uwekezaji katika nyanja mbalimbali umefikia kiasi cha shilingi trilioni 9.29,” ameongeza.

Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara awaandikie barua waajiri wote wanaodaiwa na shirika hilo na kuwataka wawasilishe fedha wanayodaiwa mara moja na wale ambao hawatalipa ndani muda utakaowekwa wafikishwe mahakamani na yeye apewe taarifa.

“Kumekuwepo na changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati hali inayoleta usumbufu mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia muda wa kustaafu. Suala hili halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa waajiri wote nchini waheshimu sheria na wawasilishe michango yao kwa wakati,” amesisitiza.

Mbali ya kuwabana waajiri, Waziri Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za shirika hilo na wapangaji wote wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na wasipofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa wafikishwe mahakamani.

“Nimeambiwa pia lipo tatizo la wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala hili lilitolewa maelekezo na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu. Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua nyumba za NSSF na bado hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini hawalipi kodi wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF ziuzwe kwa watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”

Akizungumzia utendaji wa shirika hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika hilo na Bodi ya Wadhamini kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa sukari nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mfuko wa NSSF.

“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari nchini. Tumeelezwa hapa kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,” amesema.

Mapema, akielezea utendaji wa shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara alisema limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh. 80,000 hadi sh. 100,000 kwa mwezi.

Alisema limeanza kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga nyumba za watumishi Dodoma ili kuendana na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado unaendelea lakini tumeshabaini kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200 hadi 300 mkoani Dodoma,” alisema.

Kuhusu uwekezaji kwenye ujenzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni, Dar es Salaam, Prof. Kahyarara alisema uwekezaji huo unalipa kwa sababu makusanyo ya tozo kwa watumiaji yamefikia asilimia 109. “Tuna uhakika kwamba fedha tulizowekeza zitarudi,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 45 za saruji ambazo ni sawa na mifuko 900 yenye thamani ya sh. milioni 15 kwa ajili ya waathirika wa tetememo la ardhi mkoani Kagera. Amepokea msaada huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel Wangwe.

Akiwasilisha msaada huo, Prof. Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani Kagera na wameamua kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali kukabiliana na maafa hayo. Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya madawati 6,000 yenye thamani ya sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali.

Waziri Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa walengwa.

Kikosi Kazi Cha Jeshi La Wananchi (JWTZ) Cha Wasili Kagera Kwa Ajili Ya Kujenga Miundombinu Iliyoathiriwa Na Tetemeko La Ardhi


Kikosi kazi cha jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ)kutoka makao makuu ya Jeshi kimewasili Mkoani Kagera kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya serekali iliyoathiriwa vibaya na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoana Kagera septemba 10 mwaka huu.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Kabambyaile Kata ya Ishozi Wilaya ya Missenyi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema kuwa kikosi hicho kinawataalamu wa fani zote za ujenzi na wamekuja na vifaa vyote vya ujenzi.

"Hiki kikosi kitafanya kazi kwa masaa 24 yaani watajenga usiku na mchana taasisi zote za umma zilizoathiriwa na tetemeko ikiwa ni pamoja na mashule na zahanati ili watoto waende shule na wagonjwa waendelee kupata matibabu"alisema.

Alisema mpaka kufikia july mwakani ujenzi wa miundombinu utakuwa umekamilika kwa robo tatu na aliwataka wananchi wawape ushirikiano maeneo yote watakayopita kujenga miundombinu ya umma.

Kiongozi wa kikosi hicho Meja Buchadi Kakura alisema kuwa kikosi hicho kimekuja Kagera kusaidia serekali ya Mkoa kurudisha miundombinu yote ya umma iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi katika hali yake ya kawaida.

"Ni vigumu kusema lini tutakamilisha ujenzi ila sisi tutafanya kazi usiku na mchana ili ujenzi huu ukamilike ndani ya muda mfupi"Alisema Meja Kakura.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salimu Kijuu(mwenye Suti)akisikiliza maelezo juu ya kikosi kazi cha askari waliokuja kujenga miundo mbinu ya umma iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi