Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willim Lukuvi akizungumza na mwananchi aliyesimamisha gari la Waziri wilayani Bunda
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willim Lukuvi akizungumza na Labani Ndege aliyelalamikiwa na Bibi Nyasasi Masige alipofika nyumbani kwa bibi huyo katika eneo la Nyasura C, wilayani Bunda
ZWaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willim Lukuvi akisikiliza kero mabalimbali za wananchi waliofika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilayani Bunda
- Waziri Lukuvi anayetembelea Mkoa wa Mara kutatua migogoro ya ardhi na kutekeleza agizo la Rais Magufuli, jana aliwaagiza watendaji wa idara ya ardhi mkoani humo kushirikiana na wenzao wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kupima upya eneo la Nyasura ‘C’
Bunda. Kilio cha Nyasasi Masige, mkazi wa Bunda mkoani Mara mbele ya Rais John Mgufuli kuhusu kuwapo kwa njama za kudhulumiwa ardhi yake, kimezaa matunda baada ya waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutua wilayani humo na kumaliza mgogoro huo.
Waziri Lukuvi anayetembelea Mkoa wa Mara kutatua migogoro ya ardhi na kutekeleza agizo la Rais Magufuli, jana aliwaagiza watendaji wa idara ya ardhi mkoani humo kushirikiana na wenzao wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kupima upya eneo la Nyasura ‘C’ ilipo ardhi ya bibi huyo na wamgawie viwanja viwili kama njia ya kumaliza mgogoro huo.
Septemba 5, 2018, kikongwe huyo alilalamika mbele ya Rais Magufuli kuwa baadhi ya watu akiwamo tajiri mmoja wilayani Bunda kwa kushirikiana na wataalamu wa idara ya ardhi walikuwa na njama za kumdhulumu ardhi yake, hali iliyofanya kiongozi huyo mkuu wa nchi kumwagiza Waziri Lukuvi kufika Mara kushughulikia migogoro ya ardhi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kumsikiliza bibi huyo, Lukuvi alisema amegundua kuwapo nia ovu wakati wa upimaji na uandaaji wa michoro ya eneo la Nyasura ‘C’.
“Haiwezekani eneo moja kukawepo na viwanja vyenye ukubwa tofauti kama ilivyokuwa katika eneo hili. Inaonyesha haya (makosa) yalifanyika makusudi kwa manufaa ya baadhi ya watu,” alisema Lukuvi.
Akionyesha kukerwa na makosa aliyoyagundua, waziri huyo aliagiza kazi ya kupima na kuweka michoro upya ya eneo hilo ifanyike na kukamilika ifikapo kesho.
“Mtengeneze mchoro mpya na mpime upya eneo hili na bibi kizee huyu apewe viwanja viwili bila kutozwa tozo ya premium ya asilimia 2.5 ya thamani ya ardhi kwa sababu hana uwezo. Zingatieni sheria kutekeleza hilo kwa kuhakikisha viwanja vyote vinalingana na nyumba yoyote isibomolewe,” aliagiza.
Anayelalamikiwa na bibi
Mmoja wa wakazi wa eneo la Nyasura ‘C’, Laban Ndege aliyelalamikiwa na bibi huyo kutaka kumpora ardhi yake, alikubaliana na uamuzi wa waziri na kutumia fursa hiyo kuwasilisha malalamiko yake ya kutopewa hati ya kiwanja licha ya kukamilisha taratibu zote pamoja na malipo.
Taarifa hiyo ilimfanya Lukuvi kuwahoji watendaji wa idara ya ardhi na kugundua kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawajapewa hatimiliki za ardhi licha ya upimaji kufanyika zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Pia waziri Lukuvi alisikiliza kero za wananchi zaidi ya 200 katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Bunda