HALMASHAURI ZATAKIWA KUINGIA MKATABA NA NHC KUJENGA NYUMBA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi amezitaka halmashauri nchini kuingia mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba na Ofisi kutokana na Shirika hilo kuwa na uzoefu wa kujenga nyumba zenye ubora na gharama nafuu.
Lukuvi aliyasema hayo tarehe 18 Machi 2019 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili na Utalii ilipotembelea mradi wa ujenzi wa nyumba 20 katika eneo la chatur Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga. Kati ya nyumba hizo, kumi ni za Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na nyumba nyingine kumi ni za Shirika la Nyumba.
Alisema, wakati wa kuingia mkataba wa ujenzi wa Nyumba au Ofisi Halmashauri hizo zinapaswa kuwa na fedha pamoja na kuandaa miundo mbinu (Maji, Umeme n.k) ili kuepuka kuchelewa kukamilisha ujenzi.
Mh. Lukuvi amelipongeza Shirika kwa kuendelea na ujenzi wa nyumba hizo licha ya Halmashauri kuchelewesha malipo kwa ajili ya ujenzi huo..
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiongozwa na Kaimu Mwenyeketi wake Shaban Shekilindi walihoji kuchelewa kwa mradi wa ujenzi wa nyumba hizo za Halmashauri lakini walielezwa hali hiyo imesababishwa na Halmashauri kuchelewesha malipo ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Nassib Mmbaga aliwaambia wajumbe wa Kamati kuwa Halmashauri yake ilichelewa kutoa fedha za ujenzi kwa wakati kutokana na kutumia fedha kujenga madarasa kufuatia kuwepo idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi ambao wana uhaba wa madarasa. Hata hivyo, Mkurugenzi huyo Mtendaji alieleza kuwa tatizo hilo lishatatuliwa na kuahidi kulipa kiasi cha fedha kilichobakia kulingana na mkataba.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa kufanya kazi kibiashara na kuacha tabia ya kufanya kazi kwa ushawishi wa mtu au kisiasa kwasasbu kwa kufanya hivyo kutapelekea kutouzika kwanyumba zinazojengwa hivyo Shirika litaingia kwenye hasara.
Mradi wa nyumba 20 uliopo eneo la chatur katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.


Kaimu Mwenyeketi wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Shaban Shekilindi mwenye shati jeupe ( wa pili kutoka kulia) akiongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya shirika la nyumba la Taifa Dkt. Sophia Kongela (wa kwanza kutoka kulia), Mkurugenzi Mkuu Dkt. Maulidi Banyani (wa pili kutoka kushoto) pamoja na Mkuu wa kitengo cha ukaguzi wa ndani wa Shirika Bw. Abdallah Migila (wa kwanza kushoto).
Mhe. Lukuvi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (wa pili kutoka kulia) pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Agelina Mabula ( mwenye reflector ya njano) wakiwa na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea mradi wa makazi uliopo katika eneo la chatur
wilaya ya Muhuza
Mhandisi Mannig Mwalwaka ambaye ndie msimamizi wa mradi huo akitoa maelezo ya mradi huo